UNRWA ni nini na kwa nini ufadhili wake umesimamishwa?
- Get link
- X
- Other Apps
Na Aine Gallagher
BBC Global Digital
Wakati nchi za Magharibi zikisitisha ufadhili kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina, baada ya madai ya Israel kwamba wafanyakazi wake wachache walishiriki katika shambulio la Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, tunaangalia kile UNRWA inafanya na jinsi inavyofadhiliwa.
UNRWA ni nini?
UNRWA inasimama kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usaidizi na Kazi kwa Wakimbizi wa Palestina katika eneo la karibu la Mashariki .
Inaendesha shule, huduma za kijamii, vituo vya afya na kusambaza misaada ya chakula kwa wakimbizi wa Palestina milioni 5.9 mjini Gaza, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, pamoja na Lebanon, Syria na Jordan.
Ilianzishwa wakati gani?
Ilianzishwa mwaka 1949 kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina baada ya kuundwa kwa taifa la Israel na vita vya mwaka 1948. Wapalestina 750,000 walikimbia au kulazimishwa kuondoka katika ardhi yao kwa kile walichokiita Nakba au "uharibifu".
Shirika hilo linasema limechangia katika "ustawi na maendeleo ya binadamu ya vizazi vinne vya wakimbizi wa Palestina".
Je linafadhiliwa vipi?
Ni michango ya hiari na ufadhili kutoka kwa nchi wafadhili.
Mfadhili mkubwa wa UNRWA ni Marekani, ambayo ilichangia dola milioni 343.9 mwaka 2022, wakati Ujerumani ilikuwa ya pili kwa ukubwa wa michango , ikichangia dola milioni 202.1. Kwa pamoja, nchi hizi mbili zinajumuisha karibu nusu ya ufadhili wa UNRWA wa dola bilioni 1.17 .
Kwa nini wafadhili wakuu wa Magharibi wamesitisha ufadhili wao?
Zaidi ya nchi 10, ikiwa ni pamoja na Marekani na Ujerumani, zimesitisha ufadhili kufuatia madai ya kijasusi ya Israel kwamba wanachama wasiopungua 12 wa UNRWA walihusika katika shambulio la Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, ambapo zaidi ya Waisraeli 1,200 waliuawa na zaidi ya 240 kuchukuliwa kama mateka kurudi Ukanda wa Gaza.
Umoja wa Mataifa umesema nini?
Siku ya Jumamosi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema wafanyakazi tisa wamefutwa kazi, mmoja amekufariki na wanajaribu kubaini utambulisho wa wengine wawili wa mwisho ambao madai yao yametolewa dhidi yao. Uchunguzi huru pia unafanyika.
Nchi ambazo zimesitisha ufadhili ni pamoja na Austria, Australia, Canada, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uholanzi na Uingereza.
Ireland, Norway na Uhispania zimesema zitaendelea kulifadhili shirika hilo.
UNRWA inafanya nini Gaza?
Ina wafanyakazi 13,000 na ni shirika kubwa zaidi la Umoja wa Mataifa Gaza. UNRWA inaendesha vituo vya matibabu na elimu, ikiwa ni pamoja na vituo vya mafunzo ya walimu na karibu shule za msingi za 300, pamoja na kuandaa vitabu vya kiada vinavyoelimisha vijana wa Palestina.
UNRWA imekuwa msambazaji mkuu wa chakula, maji na makazi kwa raia wa Gaza wakati wa mgogoro.
Hali iko vipi tangu kuanza kwa vita vya Israel na Gaza?
Zaidi ya watu milioni 2.3 wa Gaza wamekimbia kusini na Wapalestina milioni moja wanakimbilia katika vituo vya UNRWA. Wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas imesema zaidi ya Wapalestina 26,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi ya anga na uvamizi wa ardhini kama njia ya ulipizaji kisasi kwa shambulio la tarehe 7 Oktoba.
Kabla ya hapo, malori 500 yalikuwa yakiingia Gaza kwa siku na sasa ni chini ya 200. Kumekuwa na picha za mara kwa mara za watu waliokata tamaa wakipanda juu ya malori ya misaada ambayo hayawezi sasa kuleta misaada. Umoja wa Mataifa unasema watu milioni mbili wanahitaji msaada wa chakula.
UNRWA pia inasema wafanyakazi wake 142 katika Ukanda wa Gaza wameuawa. Kamishna Mkuu Philippe Lazzarini ametoa taarifa yenye maneno makali juu ya kupunguzwa kwa fedha. "Wapalestina wa Gaza hawakuhitaji adhabu hii ya pamoja," alisema. "Hii inatutia doa sisi sote."
Je Israeli imesema nini?
Mpaka sasa BBC haijaona taarifa za kijasusi za Israel. Ripoti katika vyombo vya habari vya Israel zinaonyesha kuwa magari ya UNRWA na vifaa huenda vilitumika katika shambulio hilo la Oktoba 7.
Mshauri wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Mark Regev, aliiambia BBC Ijumaa kwamba mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba ya Hamas yaliwahusisha "watu ambao wako kwenye mishahara yao [UNRWA]". Bwana Regev pia alimtaja mateka wa Israel ambaye, alipoachiliwa huru, alisema "alizuiliwa katika nyumba ya mtu ambaye alifanya kazi na UNRWA".
Comments