Marekani yaidhinisha mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa Iran nchini Syria na Iraq
- Get link
- X
- Other Apps
Marekani imeidhinisha mipango ya mfululizo wa mashambulizi dhidi ya malengo ya Iran nchini Syria na Iraq, maafisa wameiambia mshirika wa BBC Marekani CBS News.
Mashambuliizi hayo yatafanyika kwa siku kadhaa, maafisa wanasema, na hali ya hewa huenda itaamuru ini lini yatazinduliwa.
Hatua hiyo inajiri baada ya shambulio la ndege isiyo na rubani kuwaua wanajeshi watatu wa Marekani huko Jordan, karibu na mpaka wa Syria, siku ya Jumapili.Marekani imelilaumu kundi la wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran kwa shambulio hilo.
Kundi la Islamic Resistance in Iraq - ambalo linaaminika kuwa na wanamgambo wengi ambao wamejihami, kufadhiliwa na kupewa mafunzo na kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran - limesema ndilo lililohusika na shambulio hilo.
Iran imekanusha kuhusika na shambulio hilo lililojeruhi wanajeshi wengine 41 wa Marekani katika kambi ya kijeshi.
Wakati maafisa wa Marekani wameahidi kujibu mashambulizi hayo ya ndege zisizo na rubani, Rais Joe Biden na maafisa wengine wamesema kuwa nchi hiyo haitafuti vita zaidi na Iran.
Makundi kadhaa yanayoungwa mkono na Iran yameongeza mashambulizi dhidi ya mashirika yenye uhusiano na Marekani na Israel tangu kuanza kwa vita vya Israel na Hamas tarehe 7 Oktoba.
Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen, kwa mfano, wameshambulia meli katika Bahari ya shamu na Ghuba ya Aden, na kusababisha mashambulizi kutoka kwa Marekani na washirika wake.
Afisa wa ulinzi wa Marekani aliiambia CBS kwamba ndege isiyo na rubani ilidunguliwa usiku kucha katika Ghuba ya Aden, huku ndege isiyo na rubani ya baharini ikipigwa na kuharibiwa katika Bahari ya shamu.
Miili ya wanajeshi watatu wa Marekani waliouawa katika shambulizi hilo inatarajiwa kurejeshwa katika kambi ya Jeshi la Wanahewa la Delaware siku ya Ijumaa. Ikulu ya White House imetangaza kuwa Rais Biden atahudhuria.
Comments