Israel na Hezbollah wakaribia kupigana, wote wakataa kurudi nyuma

 

.

CHANZO CHA PICHA,AFP

Maelezo ya picha,Wanajeshi wa Israel

Vita kamili kati ya Israel na Hezbollah vitasababisha "janga", Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema. Lakini kwa David Kamari, ambaye anaishi chini ya moto unaokaribia kila siku upande wa mpaka wa Israel, vita hivyo vitakuwa suluhu.

Mwezi uliopita, roketi ya Hezbollah iliyorushwa kutoka Lebanon ilitua kwenye bustani yake katika mji wa mpakani wa Kiryat Shmona, na kupasua nyumba yake katika maeneo kadhaa na kuijaza na vifusi.

Anaonyesha mashimo ambayo vipande vya misumari vilipita kwenye kuta, vikimkosa kwa inchi chache. Na kisha kwenye vilima vilivyo juu yetu, ambapo eneo linalodhibitiwa na Hezbollah linaanzia.

"Kila siku, kila usiku: mabomu. [Ni] tatizo," alisema. "Na mimi nilizaliwa hapa. Ikiwa unaishi hapa usiku mmoja, utakuwa na wazimu."

David bado anaishi katika nyumba yake iliyojaa vifusi, vipande vya misumari vilivyonaswa na mabaki ya televisheni yake. Nje ni masalio meusi ya gari lake, lililochomwa na moto uliopita kwenye yadi yake ya mbele baada ya roketi kuanguka.

Idadi kubwa ya wakazi wa Kiryat Shmona walihamishwa baada ya mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas, huku makombora ya Hezbollah yakishambulia kumuunga mkono mshirika wao wa Palestina.

Daudi ni mmoja wa watu wachache waliobaki nyuma. "Nimeishi hapa miaka 71," alisema. "Sitakwenda. Nilikuwa jeshini, siogopi."

Suluhu yake? "Vita na Hezbollah; kuangamiza Hezbollah," anasema.

Israel imekuwa ikipiga hatua kali dhidi ya Hezbollah, na kuwaua makamanda wakuu na kulenga shabaha zaidi ndani ya Lebanon.

Hezbollah imetuma misururu mikubwa ya ndege zisizo na rubani na makombora kuvuka mpaka mwezi huu, na vitisho kwa pande zote mbili vimeongezeka.

Mapema wiki hii, kundi hilo lilichapisha picha za ndege zisizo na rubani za mitambo ya kijeshi na miundombinu ya kiraia katika mji wa Haifa wa Israel.

Mazungumzo magumu kwa muda mrefu yamekuwa sehemu ya mkakati wa kuheshimiana huku pande zote mbili zikionekana kuwa na wasiwasi wa vita kamili.

Lakini wakati mzgogoro huo ukiendelea, na zaidi ya Waisraeli 60,000 wakisalia kuhamishwa kutoka kwa makazi yao kaskazini, kuna dalili kwamba viongozi wa Israeli na raia wake wako tayari kuunga mkono mpango wa serikali kuisukuma Hezbollah ili kurudi kwenye mpaka kwa nguvu.

Meya wa Kiryat Shmona, Avichai Stern, ananionyesha eneo ambalo roketi iligonga barabara karibu na ofisi yake wiki iliyopita.

"Sidhani kama kuna nchi yoyote duniani ambayo inaweza kukubali mashambulizi ya kila siku dhidi ya raia wake," Meya Stern alisema.

"Na kukaa hapa kama wana-kondoo wa kuchinjwa, tukingojea siku ambayo watatuvamia kama tulivyoona kusini, hiyo haikubaliki.

Kila mtu anaelewa kuwa chaguo ni kati ya vita sasa au vita baadaye."

Mkwamo hatari hapa unategemea zaidi vita ambavyo Israel inapigana zaidi ya maili 100 (160km) kusini mwa Gaza.

Kusitishwa kwa mapigano huko kutasaidia kutuliza mvutano kaskazini, lakini Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu anaendelea na migogoro yote miwili, akitaka kutimiza ahadi yake kwa washirika wa serikali ya mrengo wa kulia kuiangamiza Hamas kabla ya kumaliza Vita vya Gaza.

Mapema wiki hii hata msemaji wa jeshi la Israel alisema lengo hili huenda lisiwe la kweli.

"Wazo kwamba tunaweza kuharibu Hamas au kufanya Hamas kutoweka linapotosha umma," Admirali Daniel Hagari aliiambia runinga ya Israel.

Upande wa mpaka wa Lebanon, ambapo zaidi ya watu 90,000 wamehamishwa, hali kati ya wale ambao wamesalia ni mbaya vile vile.

.
Maelezo ya picha,Mali ya David imeshambuliwa na milipuko ya roketi: "Ikiwa unaishi hapa usiku mmoja, utakuwa mwenda wazimu.

Fatima Belhas anaishi maili chache (7km) kutoka mpaka wa Israeli, karibu na eneo la Jbal el Botm.

Katika siku za awali, angetetemeka kwa hofu wakati Israel ilipolipua eneo hilo, anasema, lakini tangu wakati huo amekubali mashambulizi hayo na hafikirii tena kuondoka.

"Nitaenda wapi?" Aliuliza. "[Wengine] wana jamaa mahali kwengine. Lakini mimi sina

.Hatuna pesa."

"Labda ni bora kufia nyumbani kwa heshima," alisema. "Tumekua tukipinga. Hatutafukuzwa katika ardhi yetu kama Wapalestina."

Hussein Aballan hivi karibuni aliondoka kijijini kwake Mays al Jbal, karibu maili 6 (km 10) kutoka Kiryat Shmona, upande wa mpaka wa Lebanon.

Maisha huko yamekuwa magumu, watu wakiishi kwa mawasiliano duni na umeme sio na uhakika, na hakuna maduka yanayofanya kazi.

Familia chache zilizosalia huko ni wazee ambao wanakataa kuacha nyumba na mashamba yao, aliambia BBC.

Lakini aliunga mkono shambulio la Hezbollah dhidi ya Israeli.

"Kila mtu kusini [mwa Lebanon] ameishi kwa miaka mingi ya uchokozi, lakini ametoka akiwa na nguvu zaidi," alisema. "Ni kupitia upinzani tu ndipo tunakuwa na nguvu."

Ingawa mzozo huu wa mpaka ni hatari kwa watu wa pande zote mbili, vita kamili vinaweza kusababisha mgogoro huo kufikia kiwango tofauti.

Baadhi ya wakazi wa Beirut wanaandaa masanduku ya mizigo na hati za kusafiria tayari, endapo kutatokea mzozo wa pande zote, na kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, alisema wiki hii kwamba hakuna eneo lolote la Israel litakalosalimika.

Hezbollah ni jeshi lenye silaha, lililofunzwa vyema, likisaidiwa na Iran; Israel, nayo ina nguvu ya kijeshi ya kisasa huku Marekani akiwa mshirika wake mkuu .

Vita kamili vinaweza kuwa vibaya kwa pande zote mbili.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisema litakuwa "janga ambalo haliwezi kufikirika".

Tatizo la Israel ni jinsi ya kuzuia roketi hizo na kuwarudisha raia wake katika maeneo ya kaskazini ya nchi hiyo yaliyotelekezwa.

Tatizo la Hezbollah ni kuzuia makombora hayo wakati mshirika wake, Hamas, anashambuliwa na majeshi ya Israel huko Gaza.

Kadiri hali hiyo inavyoendelea, ndivyo hatari za hesabu zisizo sahihi zinaongezeka, na ndivyo serikali ya Israeli inavyozidi kushinikizwa kutatua hali hiyo.

Mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba yalibadilisha hesabu za masuala ya usalama nchini Israel.

Wengi wa wale walio na nyumba karibu na mpaka - na baadhi ya wale walio na nyadhifa - wanasema aina ya makubaliano yaliyofanywa na Hezbollah huko nyuma hayatoshi tena.

.

CHANZO CHA PICHA,EPA

Tom Perry anaishi kibbutz Malkiya, karibu kabisa na uzio wa mpaka wa Lebanon. Alikuwa akitoka kunywa pombe na marafiki zake wakati roketi ya Hezbollah iliposhambulia mbele ya nyumba yake mapema mwezi huu.

"Nadhani onyo la Katibu Mkuu ni sawa - vita vitakuwa janga kwa eneo hili," alisema.

"Lakini kwa bahati mbaya inaonekana kama hatuna chaguo lingine. Hakuna makubaliano yanayodumu milele, kwa sababu wanataka kutuangamiza. Tutaendelea na vita kwa muda mrefu , isipokuwa tu iwapo Israel inaweza kuiondoa Hezbollah."

Viongozi wa Israeli walipoteza uaminifu wote baada ya mashambulizi ya Oktoba 7, anasema, na hawana mkakati wa kuleta amani.

"Wanahitaji kuondoka - wote. Kufeli kwa jeshi letu na nchi yetu ilikuwa Oktoba 7, na walikuwa viongozi wetu. Hatuwahitaji viongozi hawa."

Mahitaji ya mabadiliko ya kisiasa huenda yakaongezeka wakati migogoro ya Israeli itaisha.

Wengi wanaamini kuwa waziri mkuu wa Israel anacheza na muda: akijipata katikati ya kusitisha mapigano Gaza na uungwaji mkono wa kupigana vita eneo la kaskazini.

SOURCE BBC SWAHILI

Comments

UWABATA TV

UWABATA TANGAZO

Kwanini ulaji wa nyama za watu katika nchi za Ulaya ulitumika kama tiba ya hali ya juu?

INSIGNIA LIMITED COMPANY

GRUMETI FUND TRUST,

Total Tanzania Careers 2021, Total Tanzania Jobs 2021

TECHNICIAN II (ELECTRICAL)